Katika hali isiyotegemewa na Watanzania wengi, Naibu Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson amesitisha kusikilizwa kwa hati ya dharula ya kujadili kufukuzwa kwa wanafunzi 7,802 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambao walipewa masaa 24 kuondoka chuoni.

Akielezea sababu ya kurudishwa nyumbani kwa wanafunzi hao waliokuwa wanachukua Diploma ya Ualimu Sayansi, Waziri wa Elimu, Dk. Joyce Ndalichako amesema sababu ni kugoma kwa walimu kuwafundisha sababu yakiwa ni madai yao kwa uongozi wa chuo.

“Sisi kama serikali hatuwezi kuingilia madai yao ni mambo ya hesabu za ndani tunachokifanya ni kusuluhisha ili walimu waendelee kundisha

“Kutokana na kuona bado kuna mgogoro kwa walimu na chuo tumeona ni vyema kuwarudisha nyumbani wanafunzi 7,802 wakati serikali inaendelea kufanya jitihada za kumaliza mgogoro uliopo na baada ya kukamilika wataendeleea na masomo,” amesema Dkt. Ndalichako.

Baada ya hapo mbunge wa Arumeru Mashariki, Mh. Joshua Nassari alimwomba Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson kutoa muda ili waweze kujadili hati hiyo ya dharula iliyotolewa na Mbunge wa Chemba, Mh. Juma Nkamia jambo ambalo Naibu Spika alisema siyo dharula na hivyo wabunge wa vyama vyote kwa pamoja kuungana na kutoka nje ya bunge.

Akizungumza baada ya kutoka nje ya bunge, Mbunge wa Bunda Mjini, Mh. Ester Bulaya amesema jambo pekee wanalohitaji kwa sasa ni bunge kutenga muda wa kujadili jambo hilo ambalo linaonekana kuwa na umuhimu zaidi kwa sasa.

“Hapa tunajadili mambo ya nchi na sasa kuna wanafunzi wengi wamesamba mjini hawana sehemu za kwenda alafu naibu spika anasema sio dharula tunachohitaji ni kujadili jinsi gani tunawasaidia wanafunzi hawa,

“Niwapongeze wabunge wa CCM leo kwa mara ya kwanza wamekubali kuungana na upinzani na kutoka nje ya bunge wakihitaji kujadiliwa hatma ya wanafunzi zaidi ya 7,000 wa UDOM ambao hawana sehemu ya kwenda,” amesema Bulaya.